
Mwalimu Longino alisema shule hizo mbili zimekuwa na tabia ya kufanya mitihani ya ujirani mwema na kuwa hiyo ni mara ya tatu. “Huu ni mwaka wa tatu, hata shule ya Tumaini huwa inakuja Arusha,” alisema. Mwalimu huyo alisema shule hiyo ilikuwa ya kwanza kimkoa mwaka 2004 na ya 20 kimkoa katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana. Wanafunzi hao waliofariki dunia walikuwa wakisoma shule hiyo ya bweni ambayo kwa mujibu wa wakazi wa Arusha ni miongoni mwa shule bora na iliyotoa mwanafunzi bora katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga alisema eneo la ajali lina kona nyingi na mteremko mkali na kwamba, kuna maeneo ambayo yamekuwa yakisababisha ajali kutokana na miundombinu yake ilivyokaa. Aliyataja eneo jingine kuwa lipo barabara ya Morogoro kwenda Dodoma linaloitwa Makunganya lina utelezi mwingi na kuwasihi madereva kuwa makini sana wakati wa mvua. Wanafunzi waliofariki ni wa darasa la saba. Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqaro alisema miili ya wanafunzi hao itaagwa katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid leo.


No comments:
Post a Comment