
Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo tarehe 27 April limezizima kwa
nderemo na shangwe pale alipotambulishwa rasmi mwanariadha Alphonce
Simbu, Mshindi wa medali ya dhahabu wa Mumbai Marathon, na moja ya
washindi wa London Marathon.
Mwanariadha
huyo ambaye pia ni balozi maalum wa DStv, alilitembelea Bunge kama
mgeni maalum wa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Harison Mwakyembe
akiambatana na muwakilishi wa DStv Johnson Mshana na maafisa kadhaa
waandamizi wa Jeshi la kujenga Taifa akiwemo Kanali K.J Mziray – Mkuu wa
Utawala na Mafunzo wa JKT
Mara
baada ya naibu spika wa Bunge Dk. Tulia Akson kumtaja Simbu, bunge
lilizizima kwa shangwe kwa muda hali iliyoashiria kuraha kubwa kwa
wabunge kuweza kumshuhudia mwanariadha huyo ambaye ni tegemeo kubwa la
Tanzania katika mashindano ya riadha ya Dunia yatakayofanyika mwezi
Agosti mwaka huu jijini London.
Baada
ya ziara hiyo, Simbu alipata fursa ya kusalimiana na Waziri mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa na kisha kuwa na
mazungumzo mafupi na Waziri Mwakyembe.
Akiongea
wakati wa kupiga picha ya pamoja na Simbu, Waziri mkuu Kassim Majaliwa
alimpongeza sana mwanariadha huyo na kusema kuwa Serikali inatambua na
kuthamini sana jitihada zilizofanywa na wadau wote katika kufanikisha
ushindi wa Simbu. Pia alimtakia kila la heri katika maandalizi na kisha
ushiriki wake katika mashindano ya Dunia yanayomkabili mwishoni mwa
mwaka huu.
Naye
Waziri mwenye dhamana ya Michezo Harison Mwakyembe ambaye ndiye
aliyemualika Simbu Bungeni, alisema kuwa wizara imekuwa ikishirikiana na
wadau kwa karibu ambapo hata wakati wa Safari ya Simbu kwenda London,
wizara ilihakikisha safari hiyo inafanikiwa. Ameonyesha kufurahishwa
kwake na vipaji vilivyopo na kusema nguvu za ziada zitawekwa ili
kuhakikisha kuwa vipaji hivyo vinaibuliwa na kukuzwa kwa manufaa ya
taifa zima.
Kwa
upande wake, Simbu alisema kitendo cha yeye kualikwa bungeni kimempa
faraja kubwa na pia alifurahi sana kuona jinsi wabunge walivyomshangilia
na kumpongeza. “Kwakweli ujio wangu bungeni umenipa faraja kubwa kuona
ni jinsi gani wabunge wote walivyofurahishwa na mafanikio niliyopata na
sifa niliyoiletea nchi. Hii imenipa sana moyo na uzalendo kwani ni
dhahiri kuwa taifa zima liko nyuma yangu na linanunga mkono kikamilifu”
alisema Simbu
Alitoa
shukrani za pekee kwa wadhamini wake DStv, pamoja na Waziri Mwakyembe
kwa jitihada kubwa anazofanya. Amesema anaamini kwa mwenendo huu yeye,
wanariadha wengine na wanamichezo wote wa Tanzania watafika mbali na
hatimaye Tanzania itakuwa kinara katika ulingo wa michezo duniani. Pia
alilishukuru Jeshi la Kujenga Taifa JKT kwa kumruhusu kufanya mazoezi na
kushiriki katika mashindano mbalimbali.
Simbu
ambaye ni miongoni mwa wanariadha bora wa Tanzania alivunja rekodi yake
aliyoiweka mwaka jana nchini Japan ya muda wa 2:09:19 na hatimaye katika
mashindano ya London Marathon mwaka huu alitumia muda wa 2:09:10 ambao
ndio muda wake bora zaidi.
Simbu ni miongoni wa wachezaji wa timu ya taifa ya riadha watakaoshiriki mbio za Dunia mwezi Agosti mwaka huu jijini London.
No comments:
Post a Comment