Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kutowachagulia vyuo wanafunzi wa elimu ya juu na kuwaacha wanafunzi hao kuchagua vyuo wanavyovitaka wenyewe.
Agizo hilo limetolewa leo, Jijini Dar es Salaam Rais Magufuli alipokuwa akizindua Mabweni mapya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa Chuoni hapo Juni, mwaka jana.
“Ninaamini kama wanafunzi wangepewa nafasi ya kuchagua vyuo wanavyovipenda wenyewe, vyuo vya Serikali kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Mzumbe vingekuwa na wanafunzi wengi sana,” alisema Dkt. Magufuli.
Aliendelea kwa kusema kuwa TCU imekuwa ikiwachagulia wanafunzi vyuo visivyo na sifa na makazi ya wanafunzi hivyo kusababisha wanafunzi hao kusoma katika mazingira magumu na wanapomaliza masomo yao hukosa ajira kutokana na vyuo hivyo kutokuwa na sifa.
Aidha, Rais Magufuli ameuagiza uongozi wa UDSM kutoza wanafunzi gharama ya shilingi mia tano(500) kama malipo ya makazi ya mabweni hayo kwa siku badala ya shilingi mia nane(800) inayotozwa kwa mabweni mengine yaliyopo chuoni hapo.
Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuwekeza katika elimu hivyo itahakikisha wanafunzi nchini wananufaika kwa kupata elimu bora kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu.
“watanzania walinichagua ili kutatua changamoto zinazowakabili na hivi ndivyo ninavyofanya kutatua changamoto hizo” alisema Rais Magufuli.
Naye, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amempongeza Rais Magufuli kwa kutoa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni hayo ambao kwa kiasi kikubwa yatatatua changamoto ya makazi iliyokuwa ikiwakabili wanafunzi wa chuo hicho.
Prof. Ndalichako amesema kuwa mabweni hayo yamejengwa kwa kipindi cha miezi 8 ambayo yatachukua wanafunzi 3840.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Rwekaza Mukandala ametoa rai kwa wanafunzi wa chuo hicho kuhakikisha wanaimarisha usalama katika maeneo ya mabweni hayo na kulinda miundo mbinu yote iliyoweka.
“Ni lazima mzingatie matumizi sahihi ya kila kifaa kilichofungwa katika majengo haya, majengo haya ni mapya na yamejengwa kwa gharama kubwa kwa lengo la kutusaidia kuondokana na changamato iliyotukabili kwa muda mrefu,” alisema Prof. Mukangala
Saturday, April 15, 2017
Home
/
HABARI
/
RAIS DKT MAGUFULI AZINDUA MAJENGO YA HOSTELI ZA WANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM LEO
RAIS DKT MAGUFULI AZINDUA MAJENGO YA HOSTELI ZA WANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM LEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment