Alexis Sanchez hatatizika kurejea kucheza vyema katika Arsenal baada ya kutoridhika wakati wa kipindi cha kuhama wachezaji kilichomalizika wiki iliyopita, meneja wa klabu hiyo Arsene Wenger amesema.
Sanchez, 28, alikaribia sana kuhamia Manchester City dakika za mwisho, lakini Wenger amesema "hana shaka kuhusu fikira na msimamo wa Alexis".
Arsenal walikuwa wamekubaliana uhamisho wake wa £60m na City lakini ilitegemea iwapo wangefanikiwa kumpata Thomas Lemar, ambaye aliamua kusalia Monaco.
"Atarejea upesi sana kucheza katika kiwango chake kizuri kabisa," amesema Mfaransa huyo.
"Soko limefungwa kwa sasa, kulikuwa na mambo mengi sana yaliyokuwa yanaendelea. Ni vigumu sana kuzungumza kuhusu hilo kwa sababu Lemar sasa yuko Monaco na lazima aangazie kucheza huko, Sanchez yuko hapa na anaangazia hapa," Wenger ameongeza.
"Mambo mengi hufanyika sekunde za mwisho ambayo huwa nayajutia. Hii ndiyo maana ninaamini kwamba wakati umefika tubadilishe sheria na tuwe tukifunga soko kabla ya msimu kuanza.
"Wachezaji hawajui hatima yao. Wako ndani au nje? Kuna wengine ambao wanachukuliwa na watu alasiri ya mechi, watu wanaotaka kuwachukua.
"Haifurahisi na kila meneja ligini anakubali kwamba ni wakati wa kumaliza suala la kuhama wachezaji kabla ya msimu kuanza. Huwezi kuwa na wachezaji wanajiandaa kucheza na kunao ambao wako nusu ndani na nusu nje."
Arsenal walianza ligi kwa ushindi wa 4-3 nyumbani dhidi ya Leicester, kabla ya kushindwa 1-0 Stoke na 4-0 Liverpool, kichapo ambacho kilimuuma sana Wenger.
Mechi yao ijayo itakuwa Jumamosi nyumbani dhidi ya Bournemouth saa kumi na moja jioni saa za Afrika Mashariki (15:00 BST).
No comments:
Post a Comment