LATEST NEWS

Thursday, September 7, 2017

Polisi wazungumzia kupigwa risasi Lissu


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amezungumzia tukio la kupigwa risasi mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, akiwaomba wananchi wenye taarifa kulisaidia jeshi hilo.

Muroto amesema leo Alhamisi kuwa wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na wameshafika eneo la tukio nyumbani kwa Lissu. “Tunaomba mwananchi wenye taarifa atusaidie. Jeshi la Polisi tumeanza uchunguzi, tumefika eneo la tukio na tunaendelea,” amesema. Kamanda Muroto amesema taarifa za awali zinaonyesha kuna gari aina ya Nissan lenye rangi nyeupe lilikuwa likimfuatilia Lissu.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana amewataka wananchi kuwa watulivu wakisubiri taarifa za Jeshi la Polisi na madaktari wanaoendelea na matibabu ya mbunge huyo, ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema. Akizungumza maendeleo ya matibabu ya mwanasiasa huyo ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma James Charles amesema Lissu yu hai na imara.

No comments:

Post a Comment

Adbox