LATEST NEWS

Thursday, September 7, 2017

WIZARA YA AFYA YALAANI MAUAJI YA WATOTO WAWILI WALIOTEKWA MKOANI ARUSHA.

Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inalaani vikali mauaji ya watoto
wawili ambao walitekwa na kukutwa wameuawa katika mkoa wa Arusha.

Wizara imepokea
taarifa ya vifo hivyo kwa simanzi kubwa na inalaani vikali mauaji hayo ambayo
yamekatisha uhai wa watoto hao katika umri huo mdogo. Mauaji na utekaji
waliofanyiwa watoto hawa ni ukiukwaji mkubwa wa Haki za Mtoto ikiwemo haki ya
Kuishi ambayo ndiyo haki kuu kati ya haki zote.

Wizara inawaasa
wazazi, walezi na jamii kuimarisha mifumo ya ulinzi wa watoto katika ngazi ya
mitaa, vijiji na jamii ili kuwa na
mifumo madhubuti katika kudhibiti ukatili unaofanywa dhidi ya watoto na
kusababisha majonzi makubwa kwa wazazi, familia na jamii kwa ujumla.

Jamii inakumbushwa
kuwa tatizo la utekaji wa watoto linahitaji juhudi za pamoja katika kupambana
nalo ili kuzifanya jamii zetu kuwa mahala salama kwa watoto wetu kuishi. Wizara
itaendelea kuimarisha Kamati za ulinzi na usalama wa Mtoto katika ngazi za
kata, vijiji na mitaa ili kuboresha huduma za ulinzi wa watoto wetu.

Aidha, Wizara
inalipongeza Jeshi la Polisi kwa jitihada zilizofanyika za kutaka kuwaokoa
watoto hao wakiwa hai, ingawa juhudi
hizo hazikufanikiwa.

Wizara inaomba
wazazi, walezi, familia, walimu na marafiki kuwa na moyo wa uvumilivu katika
kipindi hiki kigumu.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini

Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

07/09/2017.

No comments:

Post a Comment

Adbox