Bondia wa Kenya Veronica Mbithe amejiondoa kwa timu ya taifa ya ndondi itakayoshiriki michezo ya Jumuiya ya Madola mwezi ujao mjini Gold Coast, Australia.
Mbithe ameajiriwa na Jeshi la Kenya hivyo basi hataweza kusafiri Australia kwa sababu mafunzo ya Jeshi yananaanza Machi tarehe 25.
Mbithe anasema haikuwa rahisi kuamua kati ya safari ya Gold Coast ama achukue kazi ya Jeshi.
"Makocha wangu, mabondia wenzangu na wazazi wamenishauri ni bora niingie Jeshi kwa sababu hapo nitakuwa na mshahara wa kila mwezi," anasema Mbithe ambaye angeiwakilisha Kenya katika uzani wa light-fly kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola.
Amejaribu kila njia kuwashawishi wakuu wa Jeshi wampe ruhusa kushiriki michezo ya Gold Coast lakini wakamweleza haiwezekani.
"Jeshi wana sheria zao na hawawezi kubalisha. Sasa itabidi niende Eldoret Jumapili kwa mafunzo ya miezi saba.
"Wameniambia nikimaliza mafunzo watanipa muda mwingi wa kufanya mazoezi nitimize ndoto yangu katika ndondi.''
Bi Mbithe ni miongoni mwa mabondia wachache waliowahi kuajiriwa kwenye jeshi la Kenya.

No comments:
Post a Comment