Leo hii 23 Machi 2018 familia ya gwiji huyu itafanya hitma kwa kumbukumbu ya marehemu baba yao, nyumbani kwa binti yake mkubwa huko KIjichi.
Historia ya gwiji huyu inaanzia siku alipozaliwa tarehe 3 Machi mwaka 1955, katika eneo la Kariakoo. Mama yake alikuwa mama wa nyumbani wakati baba yake alikuwa na shughuli za uchapishaji.
Maisha yake ya utoto yalikuwa ya kawaida ila alikuwa kipenda sana uimbaji wa Tabu Ley na mwimbaji mmoja wa Guinea Sorry Kandia.
Alisoma shule ya Msingi
ikiambatana na elimu ya Madrasa. Mwaka 1970 Akiwa bado shuleni, utaona
umri wake ulikuwa miaka 15 tu, alijiunga na STC Jazz, ikiwa chini ya
mpiga gitaa maarufu wakati huo Raphael Sabuni, kabla ya hapo bendi hii
ilikuwa unajulikana kama The Jets.
Katika bendi hii
Marijani aliweza kutoka nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza ambapo
alikwenda Nairobi na kurekodi nyimbo zilizotoka katika label ya
Phillips., hili jambo la mwanafunzi kusafiri na bendi likaleta shida na
kwa vile STC ilikuwa mali ya umma akaachishwa kazi na mwaka1972
alijiunga na The Trippers ya David Mussa ambayo kwa wakati huo ilikuwa
inapiga zaidi nyimbo za hoteli na za kukopi na muimbaji wao kiongozi
wakati huo alikuwa Ali Rajabu.
Hapa ndipo ubora wake
ulifunguka haswa na kuweza kuinyanyua Trippers, ambayo sasa ilibadili
jina na kuwa Safari trippers kutokana na msimamo wa serikali wakati huo
wa kutaka majina ya nyumbani yatumike bala ya yale ya kigeni na kuwa
moja ya bendi maarufu za wakati huo. Waliweza kutoa vibao vilivyopendwa
mfululizo na kuweza kuzunguka nchi nzima.
Vibao kama Rosa nenda
shule, Georgina,Mkuki moyoni, viliweza kuuza zaidi ya nakala 10000 za
santuri na hivyo kuwezesha bendi kuwa na vyombo vyake vizuri. Bendi
wakati huo ikiwa na wanahisa wanne, ambao kwa bahati mbaya wakati bendi
ndio iko juu, wakakosa kuelewana na ukawa ndio mwisho wa bendi hiyo.
Marijani alishiriki
kutunga, kuimba nyimbo karibu zote za Trippers sanjari na kupiga gitaa
kwa baadhi ya nyimbo. Mfano wimbo Olila ambao alipiga rhythm na kuimba.
Mwaka 1976, Marijani na baadhi ya wanamuziki wa Trippers waliamua kuihama bendi na kwenda baadaye kuasisi Dar es salaam International chini ya umiliki wa Mzee Zakaria Ndabemeye ambaye bado yu hai hadi sasa.
Baadhi ya wanamuziki hao
ni pamoja na Abel Baltazar kutoka Msondo, Kassimu Mponda kutoka
Trippers, Abdallah Gama, Joseph Mulenga, Haruna Lwali na George Kessy
Omojo waliokuwa wanapiga muziki Magot pale, Said Mohamed kutoka Polisi
Jazz, Cosmas Chidumule kutoka Urafiki, Belesa Kakere kutoka Biashara
Jazz, Joseph Bernard kutoka Trippers, Ali Rajabu kutoka Trippers, na
King Michael Enock kutoka Dar es salaam Jazz.
Akiwa Dar Inter
alishiriki kutunga nyimbo mbili, Betty na Sikitiko. Hata hivyo kama
waswahili wanavyosema mafahari wawili hawakai zizi moja ndivyo
ilivyotokea kati yake na Abel Balthazal kiasi cha hatimaye Marijani
kufukuzwa ndani ya bendi kutokana na ubishi kuhusu wimbo aliotunga
Marijani, kuna maelezo kuwa wimbo ulionekana unafanana na wimbo fulani
toka Kongo na hivyo Marijani akatakiwa aubadilishe na ndipo ugomvi
ukaanza.
![]() |
MOJA YA ALBUM KALI ZA JABALI |
Hata hivyo mwishoni mwa
mwaka 1978, Marijani alirejeshwa tena kundini kutokana na rundo la
wanamuziki wa Dar Inter kuihama bendi kwa kishindo kikubwa na kwenda
kuifungua bendi mpya kabisa ya Orchestra Mlimani Park.
Aliporejeshwa Marijani
alikuja na wanamuziki wengi wapya wakati huo kama akina Christopher
Kasongo, Mohamed Tungwa, Mafumu Bilal, Hamis Milambo, Athuman Momba,
Mzee Alex Kanyimbo na wengine na kuja na mtindo wa Super Bomboka.
Katika kudhihirisha
hasira zake kwa Abel, Marijani alimtungia Abel wimbo wa kumnanga ukiitwa
Kidudu mtu ambao hata hivyo RTD waliukataa kuurekodi, jambo lililokuwa
kawaida enzi hizo kwa redio kukataa wimbo.
Sifa nyingine ambayo
Marijani alikuwa nayo ni kuibua wanamuziki chipukizi kama alivyofanya
mwaka 1983 alipomuibua kutoka Tanga kijana Mkuu Waziri Kungugu Kitanda
Milima almaaruf Fresh Jumbe ambaye kwa hakika kabisa Marijani hakujutia
kumchukua kijana huyo. Alimuamini kupita maelezo kiasi kwamba wakati
mwingine alikuwa akimuachia bendi aongoze na yeye anapumzika nyumbani.
JABALI LA MUZIKI |
Mbali na Fresh,
wanamuziki wengine ni kama vile Tino Masinge, Mohamed Mwinyikondo, Juma
Choka na wengine kibao. Ni vizuri kuelezea hapa kuwa kadri ya maelezo
yake mwenyewe marehemu baada ya kurekodi Zuena na Mwanameka na nuimbo
nyingine katika album hiyo alichoambulia ni malipo ya nauli toka RTD ya
sh 2500/- tu. Kilichosikitisha zaidi ni kuwa nyimbo zao tisa ziliuzwa
kwa kampuni ya Polygram bila ridhaa yao.
Hata hivyo safari ya Dar
International ilikoma mwaka 1987 kutokana na sababu za kawaida za kufa
kwa bendi lakini kubwa ni uchakavu wa vyombo. Hata hivyo Marijani
aliendelea kufanya muziki na kwa kipindi kifupi amewahi kucheza na
Kurugenzi ya Arusha na Mwenge Jazz ambayo alirekodi nayo wimbo mmoja wa
Ukimwi na hata kupitia bendi ya Watafiti ambayo hatimae ilikuja kuwa 38.
Mwaka huohuo wa 1987
Marijani na Muhidin Maalim Gurumo waliliongoza kundi la wanamuziki zaidi
ya 50 kutunga nyimbo maalum hasa kwa maadhimisho ya miaka 10 ya CCM na
20 ya Azimio la Arusha. Naizungumzia Tanzania All Stars. Aidha mwaka
1994 aliwahi kurekodi zong zing na marehemu Eddy Sheggy.
Bendi yake ya mwisho
ilikuwa ni Africulture ama Mahepe Ngoma ya Wajanja, iliyokuwa mali ya
Rogers Malila, alikokuwa na wanamuziki kadhaa kama akina Hassan
Kunyata, Mgosi na wengine.
SHUKRANI http://tanzaniarhumba.blogspot.com/ KWA MAKALA HAYA
No comments:
Post a Comment