Mwenyekiti wa CHAUMMA, Hashim Rungwe amemtaka Waziri wa Katiba na
Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe kuacha kuingilia mambo yanayohusu chama
cha wanasheria Tanganyika (TLS) hasa kwenye suala uchaguzi wa kumsaka
Rais wa chama hicho
Akijibu maswali ya wananchi kwenye kipindi cha KIKAANGONI
kinachorushwa katika ukurasa wa Facebook EATV, Mh. Rungwe amesema kuwa
TLS ina utaratibu wake wa kuendeshwa na kamwe haiwezi kupelekwa kama
jinsi waziri anavyotaka kwani chama hicho kinaongozwa kwa sheria na
kanuni.
“Yeye kama Waziri maoni yake ni muhimu, lakini anasema vijana
hawa wawili wana maoni ya kisiasa yaani Lissu na mwenzake lakini wakati
huo huo yeye ni waziri na mpaka amefika hapo yupo ndani ya chama cha
kisiasa. na amevaa kofia mbili. TLS haiwezi kuendeshwa kama anavyotaka
yeye, huwezi kutengeneza utaratibu nje ya utaratibu. Tuheshimu pia
taaluma za watu.” Rungwe alifunguka.
Aidha Rungwe ambaye pia ni Wakili wa Mahakama Kuu na Mwanachama wa
chama hicho ameongeza kuwa katika chama hicho hakuna sheria ambayo
inamzuia mwanasiasa yoyote kugombea nafasi na kuongeza kwamba kuwazuia
upinzani wakati waliomo kwenye chama tawala wanaruhusiwa ni kutengeneza
chuki ndani ya jamii na nchi kwa ujumla
“Kutengeneza chuki kwa makusudi it’s a great crime, hasa chuki
ikitengenezwa na viongozi waliopo madarakani, ambao wamepewa dhamana ya
kuwaongoza wananchi yeye atuache na TLS yetu, kama itaonesha watu hawa
hawaruhusiwi kugombea basi watazuiliwa kwasababu watu wanaochuja
wagombea ni sisi wenyewe”. Amesema
Hivi karibuni Waziri huyo wa Sheria na Katiba alinukuliwa akisema
kuwa serikali haiwezi kuona (TLS) ikinajiingiza katika siasa na kuongeza
kuwa kama wanataka hivyo, basi serikali haitasita kuifuta Sheria ya TLS
Sura ya 307 iliyoanzisha chama hicho cha wanasheria.

No comments:
Post a Comment