LATEST NEWS

Thursday, March 23, 2017

Masogange atakiwa kuheshimu masharti ya mahakama


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa upelelezi katika kesi ya matumizi ya dawa za kulevya inayomkabili msanii Agnes Gerald Waya maarufu kama Deal ama Masogange (28) bado haujakamilika.

Kesi hiyo imekuja leo kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Wilbard Mashauru lakini wakati ikiahirishwa mshtakiwa Masogange alikuwa hajawasili mahakamani hapo. "mheshimiwa kesi leo imekuja kwa ajili ya kutajwa, upelelezi bado haujakamilika na mshtakiwa hayupo" amesena wakili wa Serikali, Adolf Mkini 

Kabla mahakama haijasema kitu,  wakili wa Masogange, Nictogen Itege aliwasilisha udhuru mahakamani hapo juu ya mteja wake kutokuwepo.

"Mheshimiwa hakimu, naomba udhuru, mshtakiwa yuko njiani anakuja mahakamani lakini amekwama kwenye Foleni Jangwani, tumekuja kwa njia tofauti" amesema Wakili Itege.

Hata hivyo, Hakimu Mashauri alimtaka mshtakiwa kuheshimu masharti ya mahakama na kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 20, mwaka huu.

Masogange anakabiliwa na mashtaka mawili ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin na Oxazepam. Anadaiwa kufanya makosa hayo chini ya kifungu cha 18 (a) cha sheria ya kupambana na dawa za kulevya namba 5 ya mwaka 2015.

Masogange anadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14,2017 katika maeneo yasiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam  alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine).

Anadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14,2017  alitumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam.

Masogange yupo nje kwa dhamana ya kuwa na  wadhamini wawili wanaoaminika.

No comments:

Post a Comment

Adbox