Serikali imesema haitavumilia wala kusita kumchukulia hatua yeyote anayevamia na kujenga katika hifadhi za miundombinu ya barabara na reli kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Karagwe, mkoani Kagera mara baada ya kukagua barabara ya Kyaka hadi Bugene yenye urefu wa kilometa 59.1, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wananchi kuacha dhana ya kuingilia miundombinu hiyo kwa imani ya kulipwa fidia na Serikali.
“Najua bado kuna watu wanaendelea kuvamia miundombinu ya usafirishaji, sasa nasema kuwa Serikali itaendelea kubomoa pasipo kulipa fidia kwa yeyote anayevunja sheria”, amesema Profesa Mbarawa.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, Waziri Profesa Mbarawa amekipongeza Kitengo maalum cha Wahandisi Washauri Wazawa (TECU), kinachosimamiwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kwa kusimamia ujenzi wa barabara hiyo kwa kuzingatia viwango na kuwataka kuendelea kuimarisha kitengo hicho ili kiweze kufikia hatua ya kujenga barabara nchini.
Aidha, amewataka viongozi wa wilaya hiyo kuwahamasisha wananchi wake kuilinda na kuitunza barabara hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu kama ilivyokusudiwa.

No comments:
Post a Comment