Monday, March 20, 2017

ZANZIBAR YASHAURIWA KUCHANGAMKIA FURSA MBALIMBALI BAINA YAKE NA SERIKALI NA MAJIMBO NCHINI INDIA

Zanzibar imeshauriwa kuchangamkia furSa mbali mbali za ushirikiano zinapokezea baina yake na Serikali za Majimbo Nchini India katika sekta za Kilimo, Biashara, Uwekezaji, Afya na huduma za Mawasiliano kutokana na Taifa hilo liliopo Barani Asia kupiga hatua kubwa ya Maendeleo kwenye Sekta hizo.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Balozi wa Tanzania Nchini India Balozi Mohamed Hija wakati akikiongoza Kikao cha matayarisho cha Ujumbe wa Zanzibar unaoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambao tayari umeshawasili Nchini humo kwa Ziara ya Kiserikali ya Wiki Moja.

Balozi Mohamed Hija alisema Zanzibar ina fursa pana ambazo bado haijazitumia katika kujitanua kimawasiliano kwa kushirikiana na Taasisi mbali mbali Duniani katika harakati zake za kujikwamua kiuchumi na kuimarisha mipango yake ya Maendeleo hasa kwenye zile Sekta zilizo nje ya Muungano.

Alisema India imebarikiwa kuwa na Taasisi na Makampuni mengi kwenye Serikali za Majimbo ambazo zinaweza kusaidia nguvu za Kiuchumi Visiwani Zanzibar iwapo mipango ya uhakika itawekwa ukiwemo utaratibu

maalum wa kufuatilia makubaliano yanayofikiwa ya pande mbili husika. Balozi Hija aliueleza Ujumbe huo wa Zanzibar kwamba Ofisi ya Ubalozi Nchini India iko tayari kuratibu masuala yote yatayohusika na mikataba au makubaliano baina na Zanzibar na Taasisi au Serikali ya Jimbo lolote Nchini humokatika uanzishwaji wa ushirikiano wa kisekta.

Alifahamisha kwamba ipo miradi inayofikia hatua ya kutiwa saini katika uanzishwaji wake lakini kinachokosekana kuibuka kwa miradi hiyo na hatimae mengine kufifia ni ukosefu wa ufuatiliaji wa miradi hiyo jambo ambalo huwavunja moyo wale wanao nia thabiti ya kusaidia.

Balozi Hija alielezea faraja yake kutokana na ujio wa Ujumbe huo wa Zanzibar Nchini India na kusema kwamba huo ni mwanzo mzuri wa kufungua njia itakayotoa mwanga kwa Zanzibar kujitanua zaidi kiuchumi Kimataifa.

Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ziara hiyo ina lengo la kutengeneza Diplomasia juu ya ushirikiano kati ya Zanzibar na India hasa katika sekta za Afya, Kilimo, Biashara na hata Utalii.

Balozi Seif alisema India imekuwa mshirika mkubwa wa Zanzibar katika Sekta ya Afya kiasi kwamba wagonjwa wengi wa Zanzibar wanaosumbuliwa na maradhi tofauti kama Moyo, Figo pamoja na magonjwa mengine hupata huduma za matibabu katika Hospitali za India.





Kaimu Balozi wa Tanzania Nchini India Balozi,Mohamed Hija kati kati akielezea fursa mbali mbali zilizopo Nchini India ambazo Zanzibar inaweza kuzichangamkia kwenye kikao cha Ujumbe wa Zanzibar uliowasili Nchini humo kwa ziara ya Wiki Moja.

Balozi Hija alikuwa akikiongoza Kikao cha matayarisho cha Ujumbe wa Zanzibar unaoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo kwenye Hoteli ya Kimataifa ya Eros – Nehru Palace iliyopo Mjini New Delhi India.


Wa kwanza Kulia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bibi Asha Ali Abdulla. Wa kwanza Kushoto ni Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Waziri asiye ya Wizara Maalum Dr. Sira Ubwa Mamboya na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga.


Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

19/3/2017.

No comments:

Post a Comment

Adbox