LATEST NEWS

Tuesday, April 4, 2017

JAJI KIONGOZI AWATAKA MAJAJI KUSHIRIKIANA KATIKA KUWAHUDUMIA WANANCHI

Na 
Lydia Churi-MAHAKAMA, ARUSHA
 

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mheshimiwa Ferdinand Wambali amewataka Majaji wa Mahakama Kuu nchini kufanya kazi zao kwa kuzingatia Maadili, kuwa waaaminifu na kushirikiana katika kuwahudumia wananchi ili kesi zimalizike kwa haraka katika
Mahakama mbalimbali.
 

Akifungua Mafunzo ya siku tano ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tazania kuhusu Uongozi katika shughuli za Mahakama leo jijini Arusha, Jaji Kiongozi amesema lengo la Mafunzo hayo ni kujadiliana kwa kina nini kifanyike ili kesi zimalizike mapema kwenye mahakama mbalimbali nchini.

Jaji Wambali alisema katika mkutano huo, Majaji watapata nafasi ya kujifunza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania wenye nguzo tatu ambazo ni pamoja na masuala ya Utawala, Upatikanaji wa haki kwa wakati na imani ya wananchi kwa Mahakama na ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za Mahakama.

Katika Mafunzo hayo pia Majaji watajadiliana ni nini kilifanyika mwaka jana katika umalizwaji wa mashauri, changamoto zilizojitokeza na nini kifanyike ili kutatua changamoto
zinazojitokeza katika utendaji wao wa kazi wa kila siku.
 

Naye Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mheshimiwa Katarina Revokati akizungumza na Waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo alisema  yamegawanyika katika makundi matatu ambapo kundi la kwanza ni la Majaji wa Mahakama ya Rufani, kundi la pili ni la Majaji Wafawidhi wa Kanda 14 za Mahakama Kuu ya Tanzania na kundi la Tatu ni la Majaji wengine wote.
 

Alisema Majai wa Mahakama ya Rufani watapatiwa Mafunzo kuhusu namna ya kutoa maamuzi ya Mahakama katika usikilizwaji wa kesi ngazi ya Rufaa, ambapo Majaji Wafawidhi watapewa mafunzo kuhusu Usimamizi wa uendeshaji wa kesi wakati Majaji wengine watapatiwa mafunzo kuhusu uongozi na usimamizi wa kuleta mabadiliko.
 

Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Benki ya Dunia ni Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania na yanalenga katika kuboresha utendaji kazi na
kuleta mabadiliko ndani ya Mahakama.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali akifungua Mafunzo ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Ukumbi wa AICC leo jijini Arusha. Mahakama inaendesha Mafunzo kwa Majaji wote wa Tanzania ambapo Majaji wa Mahakama ya Rufani wanahudhuria Mafunzo kuhusu namna ya kutoa maamuzi ya Mahakama katika usikilizwaji wa kesi ngazi ya Rufaa, Majaji Wafawidhi kuhusu Usimamizi wa uendeshaji wa kesi wakati Majaji wengine wanapatiwa mafunzo kuhusu uongozi na usimamizi wa kuleta
mabadiliko.

No comments:

Post a Comment

Adbox