Mwacha mila ni mtumwa walisema, na wahamiaji wengi hukumbwa na changamoto ya kupoteza lugha yao ya asili.
Ingawa Kiswahili ndio lugha kuu ya asili kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika, wataalamu wa lugha wanasema Tanzania ina utajiri wa makabila zaidi ya 120, lakini yapo katika hatari ya kupoteza lugha za asili kwa kuwa idadi kubwa ya wazazi wanapuuzia lugha zao na kuwafundisha watoto lugha ya Kiswahili pekee.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), lugha za asili ni utambulisho wa makabila mbalimbali duniani na zina umuhimu mkubwa katika jamii.
Lugha za asili ndio zinazoifanya Tanzania kuwa na makabila zaidi ya 120 yenye mila, desturi na utamaduni tofauti.
Watanzania wanapaswa kuweka mikakati ya kuwaridhisha watoto lugha na utamaduni wa asili kwa kuwa ipo tofauti kubwa kati ya ukabila na makabila. Lugha na utamaduni wa asili ni urithi usioshikika na una thamani kubwa kwa Taifa hivyo wazazi wasipuuze lugha zao za asili kwa kisingizio cha kuepuka ukabila.
Wakati wa kupigania Uhuru wa Tanganyik,a Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere alihimiza matumizi ya Kiswahili ili kuimarisha mfumo wa mawasiliano na kujenga Taifa lenye nguvu na jambo hilo haliwazuii Watanzania kuendeleza makabila yao.
Makabila na ukabila Baba wa Taifa alikuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya ukabila ili kudumisha amani, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania jambo linalowawezesha Watanzania kuishi kama ndugu bila kujali tofauti za rangi, kabila wala itikadi za kidini.
Hata hivyo, Kiswahili hakipaswi kuchukuliwa kama tishio kwa lugha za asili kutokana na ukweli kuwa binadamu ana uwezo wa kujifunza na kuzungumza lugha zaidi ya tatu ikiwa ni pamoja na kudumisha mila na desturi za asili ya Afrika.
Source:Michuzi
No comments:
Post a Comment