LATEST NEWS

Monday, April 3, 2017

MIFUKO YA HIFADHI KUJENGA VIWANDA 25 NCHINI, KUZALISHA AJIRA ZAIDI YA 114000


ZAIDI ya miradi 25 inatarajiwa kutekelezwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Nchini kama sehemu ya kushiriki katika ujenzi wa Uchumi wa viwanda Nchini.
 

Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Nchini, Meshach Bandawe (pichani) wakati alipokuwa akiwasilisha mada ya ushiriki wa Mifuko ya Hifadhi katika Ujenzi wa uchumi wa Viwanda katika mkutano wa wanachama na wadau wa Mfuko wa PPF uliofanyika Jijini Arusha hivi karibuni.

Bandawe alisema kuwa Miradi hiyo itahusu viwanda vitakavyotekelezwa na Mfuko mmoja mmoja pamoja na Viwanda vitakavyotekelezwa na Mifuko yote kwa pamoja kupitia Umoja wao wa TSSA (Tanzania Social Security Association).
 

"Viwanda hivyo ambavyo vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, inajumuisha baadhi ambavyo vimeanza uzalishaji na vingine vipo katika hatua za kufanyiwa upembuzi yakinifu ambavyo kati ya hivyo vipo ambavyo vilisimama uzalishaji ambavyo vitahitaji kufufuliwa, vipo ambavyo vilikuwa vikisuasua katika uzalishaji na uendeshaji ambavyo vitahitaji kuendelezwa na vingine vitajengwa upya". alisema Bandawe.

Alivitaja Baadhi ya Viwanda hivyo kuwa ni Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi na Mbigili, viatu Karange Moshi, Vinu vya NMC Iringa, Dodoma na Mwanza, Viuadudu Kibaha, General Tyre Arusha, Chai Mponde, Nguru Ranch Morogoro, Mvinyo na Juisi ya Zabibu Dodoma, Kilimanjaro Machine tools, Tandahimba na Newala Cashewnut Union, sukari ya sweetner Tanga, Kilimo cha Wanga Lindi, Kiwanda cha Madawa TPI, Chai Kagera, Morogoro Canvas, Urafiki Dar es Salaam, Vunu vya kuchambulia pamba vya Nyanza Cooperative Union, Viwanda vya Ngozi na bidhaa za Ngozi nk.
 

Viwanda hivi ambavyo vina mnyororo mrefu wa uogezaji thamani vitategemea mali ghafi kutoka ndani ya Nchi, vitahusu pia bidhaa zinazotumiwa na watu wengi kwa ajili ya soko la ndani na Nje ya Nchi, vitatengeneza ajira nyingi na hivyo pia kupanua wigo wa wanachama wengi watakaojiunga na Mifuko hiyo na baadae kuimarisha uchumi wa Nchi.

Uwekezaji huu wa viwanda utakuwa wenye tija kwa wanachama, mifuko na taarifa kwa ujumla na miradi yote itafanyiwa upembuzi yakinifu ili kuhakikisha usalama wa fedha za wanachama na itafuata kanuni taratibu na miongozo mbalimbali ya uwekezaji na wataalam watatumika katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Viwanda hivi vitakapokamilika vinategemewa kuzalisha ajira zaidi ya watu 114,000 Nchini.

Umoja a Mifuko ya Hifadhi unaundwa na Mifuko ya NSSF, PPF, LAPF, PSPF, GEPF, NHIF, WCF na ZSSF uliopo Zanzibar.

Source:Michuzi

No comments:

Post a Comment

Adbox