Kundi la meli za kivita za
Marekani, ikiwemo meli yenye uwezo wa kubeba ndege za kivita, hazikuwa
zinaelekea upande wa Korea Kaskazini kama ilivyoripotiwa awali, bali
zilikuwa zinaelekea eneo tofauti.
Wiki iliyopita, Rais Trump pia alitangaza kwamba kundi kubwa la meli za kivita lilikuwa likitumwa eneo hilo.
Lakini imebainika kwamba ukweli ni kuwa meli hizo zilikuwa zinaelekea eneo tofauti.
Kufikia mwishoni mwa wiki, zilikuwa zimesafiri mbali sana na rasi ya Korea na zilikuwa zinapitia mlango wa bahari wa Sunda kuingia katika Bahari ya Hindi.
Wakuu wa jeshi la wanamaji la Marekani katika Bahari ya Pasifiki walisema Jumanne kwamba walikuwa wamefutilia mbali safari ya meli hizo katika bandari ya Perth.
Hata hivyo, wanajeshi wake walikuwa wamekamilisha mazoezi ya pamoja ya kijeshi yaliyokuwa yamepangwa awali kati ya majeshi ya Marekani na Australia katika pwani ya kaskazini magharibi mwa Australia.
Baada ya mazoezi hayo, meli hizo zilielekea Singapore tarehe 8 Aprili.
Kundi hilo la meli sasa "linaelekea Magharibi mwa Pasiki kama lilivyoamrishwa".
Mwandishi wa BBC anayeangazia habari za Korea Stephen Evans anasema bado haijabainika iwapo kulitokea suitafahamu katika mawasiliano au labla Marekani ilipotosha watu makusudi kujaribu kumtia wasiwasi kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un.
Awali, Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence alionekana kutoyumba alipohutubia wanahabari akiwa kwenye meli ya kivita ya USS Ronald Reagan ambayo imetia nanga Japan.
Aliapa kwamba Marekani iko tayari "kushinda shambulio lolote na kukabiliana na matumizi yoyote ya silaha za kawaida au za nyuklia kwa nguvu zake zote."
Korea Kaskazini na Marekani zimekuwa zikijibizana vikali viki za hivi karibuni na safari ya meli hizo ilikuwa imeibua uwezekano wa Marekani kutekeleza shambulio la mapema kujaribu kulemaza mfumo wa kijeshi wa Korea Kaskazini.
Jumatano, Bw Pence alitaja taifa hilo kuwa "tishio kubwa zaidi na la dharura kwa amani na usalama" katika maeneo ya Asia na Pasifiki.
No comments:
Post a Comment