Msajili wa vyama vya Siasa, Jaji Francis Mtungi, amesema kuwa amesoma katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu vurugu zilizotokea Jumamosi katika hoteli ya Vina, Mabibo Dar es salaam, zinazosemekana kuhusisha wanachama wa CUF.
Katika taarifa yake aliyoitoa leo, amesema “Ni ukweli usiopingika kwamba, suala la mgogoro wa uongozi katika chama cha CUF lipo mahakamani, lakini nikiwa msimamizi wa Sheria ya Vyama vya Siasa na kutambuliwa na jamii kuwa ni mlezi wa vyama vya siasa, nimelazimika kuwasihi wadau wa siasa hususani wanachama wa chama cha CUF, kutambua kwamba, kuwapo kwa shauri mahakamani siyo fursa ya kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani, kwani jambo hili ni uvunjifu wa sheria na linaleta sura mbaya kwa jamii.”
“Hivyo, nina laani vurugu hizo, ambazo zilionekana kuvunja amani na utulivu na watu kuumizwa, tofauti na tunu zetu za taifa za amani na utulivu. Pia, nawaasa wanachama wa CUF pamoja na tofauti walizonazo, madhali masuala haya yapo mahakamani hebu tuheshimu utawala wa Sheria,” amelaani Jaji Mutungi.
“Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na hata Jeshi la Polisi lipo kushughulikia malalamiko yoyote yanayohusu uendeshaji na shughuli za chama chochote cha siasa. Hivyo, hakuna haja ya wanachama wa chama cha CUF kukiuka taratibu za kuendesha chama hicho au kujichukulia Sheria mkononi.”
‘Aidha, nina viasa vyama vya siasa kuelewa kuwa havipo juu ya Sheria, vinapaswa kuheshimu na kufuata Sheria za nchi, ikiwamo kutunza amani na utulivu tulionao.’
Jaji Mutungi ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama katika nchi yetu kulifanyia kazi tukio hilo, ili wahusika wafahamike na kuchukuliwa hatua za kisheria. Kwa upande wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inayosimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, haitasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria.
No comments:
Post a Comment