Abedinego Damian aka Belle 9 amepata msiba mzito. Baba yake mzazi amefariki dunia usiku wa kuamkia leo. Meneja wake, Jahz Zamba, ameiambia Bongo5 kuwa Mzee Damian amefariki dunia baada ya kugongwa na boda boda iliyokuwa kwenye mwendo mkali huko mjini Morogoro alikokuwa anaishi.
Alivunja mguu mmoja pale pale na kujeruhiwa vibaya kabla ya kupelekwa hospitali. Dereva wa boda boda naye ameumia vibaya ikiwemo kuvunjika taya na kujeruhiwa kichwa. Jahz amesema baada ya Mzee Damian kupelekwa hospitali na kuwekwa kwenye wodi ya wagonjwa mahtuti, kuna dawa zilikuwa zikihitajika lakini zilikosekana kwenye hospitali hiyo. Amesema kaka yake Belle anayeishi Morogoro aliingia mtaani kuzisaka na aliporudi mida ya saa sita usiku alikuta Mzee ameshafariki.
Ni pengo kubwa kwa Belle 9 kumpoteza baba yake kwakuwa mara nyingi hudai baba yake ni mwalimu muhimu katika maisha yake. Muimbaji huyo anayetokea Morogoro alimtaja mzazi wake huyo kuwa ni mtu anayemuinspire kwa mengi.
“Mfano hai ni kwamba mpaka leo hii hapa, baba yangu bado yupo na mama yangu ni kitu ambacho nakuwaga proud,” alisema kwenye kipindi cha Ngaz Kwa Ngaz cha Salama Jabir.
“Ninavyorudi nyumbani, baba yupo, mama yupo sababu nina rafiki zangu wengi ambao wako na mama zao peke yao wengine wako na baba zao peke yao, so kwangu mimi baba yangu ni mwalimu katika hilo,” aliongeza.
Pia Belle aliwahi kukiambia kipindi cha The Playlist cha Times FM kuwa couple anayoikubali zaidi ni ya wazazi wake. “Baba yangu na mama yangu,” alijibu muimbaji huyo.
“Wananivutia kwasababu nyumbani maisha ni ya kawaida lakini still baba yuko na mama halafu mara zote ambazo nimekuwa nyumbani, sijawahi kuona mama yangu anagombana na baba. Mimi nimekaa sana nyumbani kwa muda mrefu, lakini mara ya kwanza naona kama wanashikanashikana hivi ilikuwa mimi ndio chanzo, yaani mama alikuwa ananitetea mimi kwasababu baba alikuwa ananinyoosha sana sasa mama alikuwa kama anaingia hivi, lakini haukuwa ugomvi,” aliongeza.
“Kiukwezi ni best couple kwangu mimi, najifunza mengi kupitia pale, inanipa nguvu nikirudi nyumbani baba yupo, mama yupo nikitoka hapo nami nakuwa nipo fast kila kitu.”
Tunampa pole Belle kwa msiba huo mzito na Mungu ailaze roho ya baba yake mahala pema peponi.
No comments:
Post a Comment