LATEST NEWS

Friday, April 21, 2017

Watu saba wafariki wakitazama mechi ya Manchester United Nigeria



Mashabiki hao walikuwa wanatazama mechi kati ya Manchester United na Anderlecht

Watu saba walifariki na wengine wengi kujeruhiwa baada ya kugongwa na nguvu za umeme wakitazama mechi kati ya Manchester United ya Uingereza na Anderlecht ya Ubelgiji nchini Nigeria.

Mashabiki wa soka walikuwa wamekusanyika kwenye kituo cha kutazama mechi kupitia runinga katika mji wa Calabar kusini mwa nchi hiyo mkasa ulipotokea.

Manchester United walishinda 2-1 kwenye mechi hiyo ya hatua ya robofainali ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa League.

Polisi nchini Nigeria wamesema watu saba walifariki na wengine 10 wakajeruhiwa na wamelazwa hospitalini ambapo mmoja yumo katika hali mahututi.


Kwa mujibu wa BBC kisa hicho kilitokea baada ya waya wa umeme kuangukia jumba na kulikuwa na watu 80 kwenye jumba hilo wakati wa kutokea kwa mkasa huo lakini baadhi walifanikiwa kuondoka bila majeraha

"Kufikia asubuhi, kulikuwa na watu 7 waliokuwa wamefariki. Kuna 10 ambao wamelazwa hospitalini na mmoja ambaye yumo chumba cha wagonjwa mahututi," walisema maafisa wa polisi.

„kwa mujibu wa taarifa tulizopata kufikia sasa, ni kwamba waya mkubwa wa umeme ambao ulikuwa karibu na jumba hilo ulianguka."

BBC Swahili

No comments:

Post a Comment

Adbox