[Sehemu ya 3 ya Hotuba ya ndugu Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto (MB) kuhusu Mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kwa mwaka 2017/18]
Mheshimiwa Spika
Kuna kijana wa kitanzania, ndugu Ben Saanane amepotea kwa zaidi ya miezi mitano sasa. Hajulikani alipo. Wazazi wake na rafiki zake wamemtafuta na kutoa malalamiko bila mafanikio. Wamefikisha taarifa kwa jeshi la polisi na wamepaza sauti bila kuchoka. Kuna nyakati suala hili lilionekana la siasa na ndio maana wengine tulikaa pembeni. Lakini sasa ni miezi 6, kuna taarifa juu ya suala hili, nimeona nisikae kimya juu ya hili.
Taarifa zinatoka chini chini, sio rasmi, kwamba huyu kijana 'ametoweshwa'. Kwamba alishikiliwa na watu wa Idara ya Usalama na amepotezwa. Jeshi la Polisi wana taarifa za mawasiliano ya mwisho ya Ben Saanane kwa kutumia simu yake ya mkononi, ambayo inaonekana simu ilipoteza mawasiliano akiwa maeneo ya Buguruni siku aliyotekwa tarehe 15/16 Novemba 2016 na tangu siku hiyo hapakuwa na mawasiliano tena.
Siku hiyo simu yake ilisoma maeneo ya Tabata asubuhi, kisha Mikocheni na Mwenge muda mwingi wa mchana. Saa mbili usiku alikuwa Mburahati na saa nne usiku ilizimwa akiwa Buguruni. Polisi wanajua kuwa wenzao wa Usalama wa Taifa ndio waliomteka kijana huyu lakini hawawezi kuchukua hatua dhidi yao. Hivyo wameamua kukaa kimya wakiamini kuwa Watanzania tutasahau.
Jambo hili linasikitisha na kuumiza sana, Ben ni kijana wa kitanzania, ni mtoto, mjomba, baba, kaka, anayo familia, siwezi hata kufikiria ni namna gani familia yake inaumia kwa miezi hii sita bila kumuona ndugu yao, bila kujua alipo, bila kujua hatma yake. Inaumiza sana, inaumiza mno, ni jambo gumu sana kulivumilia, si jambo rahisi kulipuuzia na kusahau tu. Watanzania hatupaswi kukalia kimya kuhusu jambo hili, tukisahau hili hakuna atakayepona.
Kumekuwa na matukio ya namna hii mabaya kabisa huko nyuma; ndugu Absalom Kibanda, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri alivamiwa na kuumizwa vibaya sana na leo jicho lake moja halioni mwaka 2013. Pia ndugu Yona wa Temeke alitekwa na kuumizwa na kutupwa huko mbweni jijini Dar es salaam na hakuna mtu yeyote aliyekamatwa juu ya matukio yote hayo. Orodha ya matukio ya namna hii ni ndefu.
Watanzania wamesahaulishwa yote haya, Polisi mpaka Leo hawajamkamata hata mtu mmoja juu ya yote hayo. Sababu kubwa ni ukimya wetu. Sisi wabunge tumepewa ridhaa na wananchi wenzetu kuyasema haya, tumepewa mamlaka ya kuihoji serikali juu ya mambo ya wananchi, na Usalama wao na mali zao ni jambo la kwanza la msingi kabisa, wananchi wetu wakiwa na mashaka juu ya usalama wao, shughuli za uzalishaji mali zitakuwa duni, uchumi wa Taifa utadorora zaidi. Tunao wajibu wa kuhakikisha Usalama wa wananchi wetu, ni wakati wa kuibana Serikali juu ya hili.
Mheshimiwa Spika,
Naomba kulikumbusha Bunge lako Tukufu na wananchi Kwa ujumla kwamba Usalama wa Taifa hawana mamlaka yeyote kisheria kukamata mtu yeyote yule Kwa mujibu wa kifungu cha 5(2) cha sheria ya usalama wa Taifa ya mwaka 1996 Kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kadhaa. Kwa hiyo Askari wa Usalama wa Taifa waliokwenda Clouds Media na silaha, Askari wa Usalama aliyemtolea silaha Mbunge wa Mtama, ndugu Nape, na kikosi cha utekaji na utesaji cha Usalama wa Taifa kinachohusishwa na utekaji wa watu wanavunja sheria ya usalama wa Taifa.
Hata askari wa Usalama wa Taifa waliomkamata Mbunge wa Geita Vijijini, ndugu Msukuma, Mbunge wa Nzega, ndugu Bashe na Mbunge mstaafu, ndugu Malima walivunja sheria ya Usalama wa Taifa. Kuna viashiria vyote kuwa hali si nzuri kabisa.
Lakini kuna jambo moja muhimu sana juu ya jambo hili, MTAZAMO HASI wa Watanzania juu ya Idara ya Usalama wa Taifa. Idara Nyeti, Muhimu na ya Kuheshimiwa mno kwa Taifa letu, inaniuma leo kusimama hapa Bungeni kuisema Idara ya Usalama wa Taifa. Mimi niko Bungeni mwaka wa 12 huu, hatuzungumzii mambo ya Usalama wa Taifa humu bungeni, jambo hilo ni 'Taboo', lakini kwa hali ilivyo sasa imenibidi niseme.
Mambo haya maovu yanayohusishwa na Idara hii yanaondoa uhalali wa Taasisi hii kwa wananchi, yanaondoa heshima, hadhi na uaminifu juu ya idara hii, yanajenga chuki na taswira hasi ya Wananchi kwa idara hii, hili si jambo jema kwa Taifa. Ni wakati sasa wa kuchukua hatua. Ni lazima Bunge liamke na kukomesha hali hii.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 120(2) ya Kanuni za Bunge natoa Taarifa kwamba nitatoa hoja binafsi kutaka Bunge lako Tukufu kuunda Kamati Teule kufanya uchunguzi kuhusu vitendo vya utekaji, uteswaji na hata mauaji dhidi ya raia (suala la Ben Saanane likiwemo).
Pamoja na mambo mengine, Kamati teule hiyo pia nitapendekeza iangalie namna ya kufanya mabadiliko makubwa kwa Idara ya Usalama wa Taifa ili kuiondoa kuwa Idara ya utesaji na badala yake kuwa idara ya kulinda Wananchi, Rasilimali za nchi na Ulinzi wa Katiba ya nchi.
Naamini wabunge wenzangu mtaniunga mkono kwenye hili.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge - Kigoma Mjini (ACT Wazalendo)
Dodoma
Aprili 11, 2017
Source:MPEKUZI
Tuesday, April 11, 2017
Home
/
BUNGENI
/
Zitto Kabwe Awatuhumu Usalama wa Taifa Kwa Kuhusika na Utekaji Wa Wananchi.......Huu ni Mchango Wake Alioutoa Bungeni
Zitto Kabwe Awatuhumu Usalama wa Taifa Kwa Kuhusika na Utekaji Wa Wananchi.......Huu ni Mchango Wake Alioutoa Bungeni
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment