Wednesday, May 10, 2017

Serengeti Boys Wapata Neema Na Uzinduzi Wa Sportpesa


Timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 kwa mchezo wa soka maarufu kama Serengeti Boys, imefanikiwa kuwa mnufaika wa kwanza wa ujio wa kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa nchini Tanzania ambayo imezinduliwa Jumanne kwenye ukumbi wa Hyatt Regency uliopo jijini Dar Es Salaam.
 
Akitangaza taarifa hiyo njema, Mkurugenzi Mtendaji wa SportPesa, Tanzania Ndugu Abbas Tarimba ameahidi kiasi cha Shilingi Milioni 50 za Kitanzania mbele ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ndugu Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo.
 
“Tunataka kuwa sehemu ya hadithi ya mafanikio ambayo SportPesa imeleta nchini Kenya. Sote tunakumbuka kuwa Kenya walikuwa nafasi za chini kwenye viwango vya ubora vya FIFA lakini tangu SportPesa itie mkono wake kwenye ligi kuu na zile za mikoa, mabadiliko makubwa yameweza kutokea.
 
“Tumekuwa tukitazama kwa jicho yakinifu mambo ambayo yamekuwa yakijiri kwa jirani zetu Kenya kwa sababu tunataka mabadiliko sawa yatokee kwa upande wa Tanzania,” alisema Ndugu Tarimba wakati akiongea na vyombo vya habari.
Sambamba na udhamini huo kwa Serengeti, Tarimba pia alisema kuwa mwishoni mwa wiki hii, SportPesa itatangaza timu za Tanzania ambazo itaweza kuingia nazo makubaliano ya udhamini.

Naye Waziri aliupokea vyema udhamini wa SportPesa kwa Serengeti akisisitiza kuwa utasaidia kuongeza ari kwa vijana chipukizi wenye vipaji kama ilivyo kwa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye anakipiga katika klabu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji.
 
“Tumekuwa tukishuhudia mambo ambayo wamekuwa wakifanya kwenye nchi nyingine na tunataka kuwapa ushirikiano ili waweze kufanikisha jitihada zao. Tunataka kuzalisha kina Samatta wengi na ukweli ni kwamba tunao kina Samatta 22 kwenye kikosi cha Serengeti ambao wanahitaji kuongezewa uwezo.
 
“Tuna furaha juu ya yale waliyoyafanya kwa upande wa Kenya na tunaamini kuwa watafanya vivyo hivyo kwa upande wa Tanzania. Ninatoa rai kwa Watanzania kuipokea SportPesa kwa mtazamo chanya na tutafanya kazi pamoja kwa ukaribu mkubwa ili tuweze kuhakikisha kuwa nchi inanufaika kutokana na uwekezaji wao” Alisisitiza Dkt. Mwakyembe
Serengeti Boys walikata tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa upande wa vijana Oktoba mwaka jana badala ya Congo Brazzaville ambao walithibitika kumchezesha mchezaji Langa Less Bercy mwenye umri mkubwa kwenye mchezo wao wa kufuzu dhidi ya Serengeti Boys.

No comments:

Post a Comment

Adbox