Ndege inayomilikiwa na kampuni ya Safari Air Link ambayo
ilikuwa ikitokea Arusha kuelekea Serengeti mkoani Mara kwa ajili ya
kuchukua abiria, ilianguka na kusababisha kifo cha mtu mmoja ambaye ni
rubani.
Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria watano ilianguka
jana katika milima ya Monduli kijiji cha Engalaon kilichopo wilaya ya
Arumeru mpakani na wilaya ya Monduli huku chanzo cha tukio hilo bado
hakijajulikana.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Omari Mkumbo alisema kwamba
ndege hiyo aina ya Cessina 206 yenye namba za usajili 5H-SAL 206 ilianza
safari ya kutoka uwanja wa ndege wa Arusha jana muda wa saa 1:05
Asubuhi ikiwa na rubani pekee na muda wa saa 4:00 Asubuhi taarifa za
kuanguka ndege hiyo zilianza kusikika.
“Mara baada ya taarifa hiyo muda wa saa 6:30 Mchana ndege
hiyo ilionekana na kubainika kuwepo kwa mwili wa mtu mmoja ambaye ni
Rubani aliyejulikana kwa jina la David Mbale (25) mkazi wa Dar es saalam
ambao umehifadhiwa katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru”. Alisema
Kamanda Mkumbo, na kubainisha kuwa uchunguzi wa tukio hilo utafanywa na
wataalamu ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment