Serikali imesema kutokana na utapeli na uuzaji holela wa viwanja eneo la Toangoma wilayani Temeke, hakuna atakayebomolewa nyumba eneo hilo.
Kauli hiyo inayotokana na agizo la Rais John Magufuli imetolewa leo Agosti 30, wakati tayari nyumba zipatazo 300 zimewekwa alama ya X kuashiria kuwa zinapaswa kubomolewa.
Akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Masaki, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema, "Rais Magufuli aliniambia hamkumchagua ili awabomolee nyumba zenu bali awaboreshee makazi na kuwaletea maendeleo."
Serikali pia, imeagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua dhidi ya watu wote waliohusika na uuzwaji wa maeneo na kufanya udanganyifu.
Wananchi kwa upande wao wametakiwa kujiepusha na ujenzi holela na kununua viwanja kwa njia isiyo halali ili kuepuka usumbufu.
Uongozi wa Wilaya ya Temeke juzi Agosti 28 uliitisha kikao na wananchi wanaodaiwa kujenga katika eneo linalodaiwa kuwa la Serikali lililotengwa kwa ajili ya kuendeleza ukanda wa kijani linalojulikana kwa jina la Bonde la Makamba.
Serikali wilayani Temeke iliwataka wananchi hao waondoke kabla ya ubomoaji kuanza.
No comments:
Post a Comment