Maofisa
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutoka makao
makuu jijini Dar es Salaam, wamewahoji kwa zaidi ya saa sita, madiwani
waliojiuzulu Chadema wanaotuhumiwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki,
Joshua Nassari kuwa walipewa rushwa.
Waliofika
Takukuru ni Catherine Mtui, aliyekuwa diwani wa viti maalumu, Japhet
Jackson (aliyekuwa diwani wa Ambuleni) na Bryson Isangya (aliyekuwa
diwani wa Maroroni). Baada ya kuhojiwa hawakutaka kuzungumza chochote
wakisema wanaacha uchunguzi uendelee.
Pamoja
nao, diwani wa Mbuguni, Ahimidiwe Rico anayedaiwa kuwa ndiye alirekodi
sauti na picha wakati akishawishiwa na viongozi wa Serikali na wa
Halmashauri ya Meru amehojiwa kwa zaidi ya saa tatu jana Jumanne Oktoba
17, 2017.
Rico
amesema amewaeleza Takukuru kila kitu ambacho anakifahamu katika sakata
hilo, ikiwemo kuwarekodi viongozi ambao walimshawishi kujiuzuru
udiwani.
"Msimamo
wangu ni kwamba, nachukia rushwa. Nimewaeleza kila kitu na wao
waliniuliza kuhusu vifaa nilivyotumia kuwarekodi nikawaambia ni mali ya
mbunge, alivitoa nchini Uingereza," alisema.
Rico
aliyesindikizwa na diwani wa Nkwanankore, Wilson Nanyaro amesema ana
imani na Takukuru kwamba watafanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua.
"Nimewaeleza
wazi kuwa hata shauri hili likienda mahakamani nipo tayari kwenda kutoa
ushahidi na kuthibitisha sauti za watu ambao niliwarekodi," alisema.
Alisema
baada ya mahojiano yaliyoanza saa tatu hadi saa sita mchana, maofisa wa
Takukuru walimwambia aondoke na watamuita watakapomuhitaji.
Hakuna
ofisa wa Takukuru aliyekuwa tayari kuzungumzia mahojiano hao wakisema
wasemaji ni makao makuu ya ofisi hiyo Dar yaliyoko jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment