LATEST NEWS

Thursday, October 12, 2017

Tume ya Uchaguzi DRC: ”Hakuna uchaguzi mpaka katikati ya mwaka 2019”

 
Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kuwa, hakuna uchaguzi utakaofanyika nchini humo hadi katikati ya mwaka 2019, hatua ambayo bila ya shaka itakabiliwa na malalamiko makubwa ya wapinzani wanaosema kuwa, rais Joseph Kabila wa nchi hiyo anafanya njama za kuendelea kubakia madarakani.

Uchaguzi huo awali ulipangwa kufanyika mwaka jana, hata hivyo uliakhirishwa kutokanana na sababu mbalimbali likiwemo suala la ukosefu wa usalama na kutokuwa tayari Tume ya Uchaguzi kuandaa uchaguzi huo kutokana na ukosefu wa bajeti. Baada ya vuta nikuvute, hatimaye kulifikiwa makubaliano ya kufanyika uchaguzi huo mwishoni mwa mwaka huu.

Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema katika taarifa yake baada ya mkutano na asasi za kiraia kwamba, itahitajia siku 504 kwa ajili ya kuandaa uchaguzi huo.

Kamisheni hiyo ya uchaguzi imesema kuwa, inatarajia kutangaza mwezi huu jedwali ya uchaguzi wa Rais na chaguzi nyingine.
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Joseph Kabila ambaye aliingia madarakani mwaka 2001 baada ya kuuliwa baba yake Laurent Desire Kabila, alishinda katika chaguzi mbili za mwaka 2006 na 2011. Kwa mujibu wa katiba, duru ya uongozi wa Kabila ilipasa kumalizika mwezi Disemba mwaka jana, ambapo asingeweza kugombea kiti cha urais kwa muhula mwingine wa tatu mfululizo.

Hata hivyo kwa mujibu wa makubaliano hayo ya mwezi Disemba mwaka jana ambayo chama cha UPDS kinasema hayana itibari tena, Kabila aliruhusiwa kuendelea kubakia uongozini hadi mwishoni mwa mwaka huu wa 2017. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kuakhirishwa tena uchaguzi huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kunaweza kuitumbukiza nchi hiyo katika machafuko ya ndani, huku tayari kukiwa na changamoto ya ukosefu wa usalama hasa mashariki mwa nchi hiyo kutoka kwa makundi ya waasi.

No comments:

Post a Comment

Adbox