
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Mwigulu Nchemba (Oktoba 17) amekagua eneo la ujenzi wa nyumba za Polisi jijini Arusha zinazoendelea kujengwa baada ya ajali ya moto iliyotokea mwishoni mwa mwezi Septemba ambayo ilisababisha familia za askari 13 kuunguliwa vitu mbalimbali na kukosa makazi.
Mwigulu alitumia fursa hiyo kwa kuishukuru kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ambayo inaoongozwa na Mkuu wa mkoa Mh. Mrisho Gambo lakini pia aliwashukuru wadau ambao wote kwa pamoja walichukua hatua za haraka za kurejesha makazi ya askari ambao walikumbwa na janga la moto huku akisisitiza kwa kusema kwamba hali ilioonyeshwa na wadau hao ni mfano mzuri wa kuigwa na mikoa mingine waone nchi inajengwa na wananchi.

Alisema Serikali ikishamaliza hilo itaendelea na utaratibu mwingine wa kujenga majengo ya kisasa ili askari wapate makazi bora huku akimuagiza Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha awafikishie salamu askari wa Arusha kwamba, Mh. Rais yupo pamoja nao na Wizara ipo pamoja nao.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo mbali na kuendelea kuwashukuru wadau hao kwa kujitolea na kumuunga mkono Mh. Rais ambaye alionyesha njia siku hiyo hiyo usiku kabla hakujapambazuka kwa kutoa mchango wake kama Serikali, lakini pia alisema bado milango ipo wazi kwa watu wengine ambao hawakuwa na taarifa juu ya tukio hilo ili kulisaidia Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha liweze kufanikisha ujenzi wa makazi ya askari hao.


Jumla ya nyumba 29 za askari katika moja ya kambi iliyoathirika na ajali ya moto zilianzwa kujengwa toka tarehe 2 mwezi huu jijini hapa na saba ambazo zipo katika ngazi ya msingi zinatarajiwa kujengwa katika kituo kidogo cha Polisi Morombo kata ya Murieti.
No comments:
Post a Comment