LATEST NEWS

Thursday, April 13, 2017

Jeshi la polisi Dar limejiandaa vyema kuipokea Pasaka






Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Kamishna Simon Sirro amesema jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limejipanga vyema kuhakikisha ulinzi na usalama unaendelea kuimarika katika sikukuu ya Pasaka.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari Kamishna Sirro alisema lengo la kuimarisha ulinzi kipindi cha Sikukuu ya Pasaka ni kuhakikisha wananchi wa jiji hilo wanasherehekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu kwa kuwa uzoefu unaonesha kuwa mara nyingi kipindi cha sherehe watu wenye nia ovu hujiandaa kufanya vitendo vya kihalifu.

Aliongeza kuwa askari polisi watafanya doria za miguu na magari katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha vitendo vyote vya kihalifu vinadhibitiwa

“Jeshi la Polisi Kanda Maalumu limejipanga kwa namna nyingi, ikiwa ni kufanya doria za saa ishirini na nne katika maeneo yote ya jiji hasa maeneo yenye viashiria vya uhalifu, pia patakuwa na doria maeneo ya makanisani, Kumbi za starehe na maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu,”alisema Kamanda Sirro.

Sambamba na hilo, askari kanzu pamoja na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), mbwa na farasi pamoja na vikosi vyote.

“Jeshi la Polisi linawaomba wakazi wa jiji kuonesha ushirikiano kwa kutambua kuwa jukumu la kuzuia uhalifu ni la kila mmoja wetu, hivyo washiriki kutoa taarifa za uhakika za kihalifu ili kuhakikisha hatua zichukuliwe haraka kabla madhara hayajajitokeza.”

No comments:

Post a Comment

Adbox