LATEST NEWS

Friday, April 21, 2017

Mke wa Marehemu bilionea Erasto Msuya Agonga Mwamba Mahakamani


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema kesi ya mauaji inayomkabili mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita (41) na mfanyabiashara Revocatus Muyela (40) ipo kihalali mahakamani hapo.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alitoa uamuzi huo jana dhidi ya hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi unaodai kesi hiyo namba 5 ya 2017 imefunguliwa kinyume na sheria ukitaka ifutiliwe mbali.

Hakimu Simba alisema upande wa utetezi unaweza kuwasilisha rufaa Mahakama Kuu kama hawajaridhika na uamuzi huo.

“Nimepitia maombi yaliyoletwa na upande wa utetezi na majibu yaliyotolewa na upande wa mashtaka, nimegundua lugha iliyotumika ni kuachia lakini Jamhuri ina uwezo wa kuwakamata tena na kuwashtaki.” alisema Simba

Wakili wa Serikali, Patrick Mwita alisema upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa. Hakimu aliiahirisha kesi hiyo hadi Mei 4.

Februari 23, washtakiwa Mrita na Muyela waliachiwa huru na Mahakama mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa kisha wakakamatwa na baadaye kusomewa mashtaka ya mauaji upya.

Kwa pamoja wanadaiwa kumuua kwa kukusudia Aneth Msuya, ambaye ni dada wa marehemu bilionea Msuya, Mei 25, 2016, eneo la Kibada, Kigamboni Dar es Salaam.

Awali, baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka ya mauaji wakili wao, Peter Kibatala aliiomba Mahakama kufuta kesi hiyo akidai imefunguliwa kinyume na sheria kwa kuwa ilishafutwa.

Alidai kesi hiyo ilifunguliwa kinyume na sheria kwa sababu ilishatolewa uamuzi Februari 23 na Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa aliyewaachia huru.

“Hakimu Mwambapa katika uamuzi wake aliwaachia huru na hawakupaswa kukamatwa na kuletwa tena mahakamani kusomewa shtaka jipya la mauaji.Bali upande wa mashtaka ulipaswa kuomba marejeo Mahakama Kuu au kukata rufaa,” alidai wakili huyo wa utetezi.

Alidai Mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kulipokea jalada jipya na kuwasomea washtakiwa mashtaka yao kwa kuwa limeshatolewa uamuzi mahakamani hapo.

Wakili wa Serikali Kishenyi Mutalemwa alipinga hoja hizo na kudai washtakiwa wamesomewa shtaka hilo kwa mujibu wa sheria na kwamba, uamuzi uliotolewa na upande wa mashtaka ulikuwa na nafasi ya kuwakamata kuwasomea shtaka hilo la mauaji.

Source:Mpekuzi

No comments:

Post a Comment

Adbox