SIMBA SC imetoka nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2 dhidi ya wenyeji, Mbao FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Sifa zimuendee mshambuliaji Muivory Coast, Frederick Blagnon aliyetokea benchi na kwenda kufunga mabao mawili dakika za lala salama kabla ya kiungo Muzamil Yassin kufunga la ushindi.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Shomari Lawi kutoka Kigoma aliyesaidiwa na Joseph Bulali na Mohammed Mkono wote wa Tanga, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika wenyeji Mbao FC wakiwa mbele kwa mabao 2-0.
George Sangija alianza kuwainua vitini mashabiki wa timu ya nyumbani kwa bao safi dakika ya 21 baada ya kuwatoka mabeki wa Simba na kuingia kwenye boksi la Simba kabla ya kumchambua kipa Peter Manyika.
Baada ya bao hilo, kocha Mcameroon wa Simba, Joseph Marius Omog alifanya mabadiliko akimpumzisha mshambuliaji Pastory Athanas na kumuingiza kiungo Said Hamisi Ndemla.
Mbao wakaendelea kutawala mchezo baada ya bao hilo na haikuwa ajabu dakika ya 36 walipopata bao la pili kupitia kwa Evarigestus Bernard aliyemalizia pasi ya mfungaji wa bao la kwanza, Sangija.
Baada ya bao hilo, kocha Omog wa Simba akamuinua mshambuliaji Mrundi Laudit Mavugo kwenda kuchukua nafasi ya beki wa kulia, Hamad Juma.
Simba wakafanya mabadiliko ya ndani, Bokungu akienda kucheza beki ya kulia na Mghana James Kotei akirudi kucheza beki ya kati na Mganda Juuko Murshid.
Kipindi cha pili, kocha Omog alikianza na mabadiliko tena akimtoa mshambuliaji Juma Luizio na kumuingiza Blagnon aliyekwenda kufanya kazi kubwa akicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi kuu mzunguko wa pili.
Blagnon alifunga bao la kwanza la Simba dakika ya 82 kwa kichwa kuparaza akiwa amelipa mgongo lango la Mbao kufuatia mpira mrefu wa James Kotei.
Bao hilo lilifungwa dakika tano tu baada ya Nahodha wa Mbao, Yussuf Ndikumana kuumia na kukimbizwa hospitali, nafasi yake ikichukuliwa na.
Blagnon tena akawainua vitini mashabiki wa Simba baada ya kufunga katika purukushani kwenye eneo la Mbao kufuatia mpira mrefu wa Bokungu dakika ya 91.
Katika mchezo huo uliodumu kwa dakika 103, kiungo Muzamil Yassin aliifungia Simba bao la ushindi dakika ya 96 akimalizia mpira uliorudi baada ya kuokolewa na mabeki wa Mbao.
Ushindi huo unairejesha Simba kileleni, ikifikisha pointi 58 baada ya kucheza mechi 26, wakati mabingwa watetezi, Yanga wanarudi nafasi ya pili kwa pointi zao 56.
Kikosi cha Mbao FC kilikuwa; Erick Ngwengwe, Asante Kwasi, David Mwasa, Boniphace Maganga, Yussuf Ndikumana, Vincent Philipo, George Sangija, Salmin Hoza, Pius Buswita, Ibrahim Njohole na Everigeston Bernard.
Simba SC; Peter Manyika, Hamad Juma, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’,
Juuko Murshid, Janvier Bokungu, James Kotei, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin, Juma Luizio, Mo Ibrahim na Pastory Athanas.
Monday, April 10, 2017
SIMBA YAREJEA KILELENI LIGI KUU KWA STAILI...YAIPIGA MABO 3-2
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment