Mahakama Kuu Agosti 16 inatarajia kusikiliza rufaa ya mbunge
wa Arusha Mjini, Godbless Lema anayepinga kushtakiwa akituhumiwa
kuhamasisha maandamano yaliyopewa jina la Ukuta, Septemba Mosi mwaka
jana.
Lema kupitia mawakili, John Mallya na Sheck Mfinanga anapinga kesi
hiyo kusikilizwa katika mahakama za chini, akitaka Mahakama ya Katiba
itafsiri kwanza vifungu vya Katiba na sheria ya vyama vya siasa. Rufaa
hiyo ilipangwa kusikilizwa jana na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha,
Modesta Opio lakini iliahirishwa kutokana na kutokuwapo mahakamani
mawakili wa Serikali, huku wa Lema wakieleza hawakuwa wamejiandaa kwa
ajili ya usikilizwaji.
Lema katika kesi hiyo anadaiwa kuhamasisha kwa
kutumia ujumbe wa WhatsApp maandamano ya Ukuta yaliyokuwa yamepangwa
kufanyika Septemba Mosi mwaka jana nchi nzima. Hata hivyo, yaliahirishwa
na viongozi wa Chadema waliokuwa wameyaandaa.
Katika rufaa, Lema
kupitia mawakili wake anaiomba Mahakama kutoa tafsiri ya ibara ya 18 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria ya vyama vya siasa.
Mawakili hao wanaeleza Katiba na sheria hiyo inampa haki kiongozi au
mwanasiasa, kufanya shughuli za kisiasa na si mtu mwingine kuwakataza au
kuingilia kati.
Katika kesi namba 352/2016 , Hakimu Mkazi Bernard
Nganga, Februari 8 alitoa uamuzi mdogo wa kutupilia mbali pingamizi la
Lema la kutaka kesi hiyo iondolewe mahakamani hapo na kuhamishiwa
Mahakama Kuu akisema kesi hiyo si ya kikatiba.
Hakimu Nganga wa Mahakama
ya Hakimu Mkazi Arusha amesema kesi hiyo ni ya jinai na mahakama hiyo
inaweza kuendelea kuisikiliza kwa mujibu wa sheria. Lema alikata rufaa
ambayo sasa itasikilizwa Agosti 16.

No comments:
Post a Comment