LATEST NEWS

Friday, August 11, 2017

Epl imerudi, Arsenal vs Leicester kufungua pazia



Msimu wa Epl mwaka 2003/2004 ilikuwa mara ya mwisho kwa vijana wa Arsene Wenger kuchukua kombe la ligi kuu nchini Uingereza na toka hapo wamekuwa wanaliona kwenye video tu.

Leo Arsenal wanafungua pazia la ligi kuu ya nchini Uingereza kwa msimu wa mwaka 2017/2018 ambapo watacheza dhidi ya bingwa wa msimu wa mwaka juzi Leicester City.

Msimu huu Arsenal wanaonekana kupania sana kurudisha heshima kwani achilia mbali wameishinda vita ya kumbakisha Alexis Sanchez bali pia wamemnunua Alexandre Lacazette.

Arsenal wamekuwa wakihangaika sana kuhusu suala la mtu sahihi wa kucheka na nyavu na ujio wa Lacazette unaonekana kama muarobaini wa tatizo hilo, na uwepo wake pamoja na Sanchez unaweza wapa Gunners kitu kipya.

Ushindi katika mechi ya ngao ya hisani dhidi ya Chelsea unawapa Guners kujiamini zaidi hii leo wanapoenda kuikabili Leicester ambao wanaonekana kikosi chao hakijatulia.

Leicester msimu huu nao mambo yanaweza kuendelea kuwa magumu kwao kwani kikosi chao ni kile kile na kochwa wao Craig Shakespare hajafanya usajili wa kutisha zaidi ya kumnunua Kelechi Iheanacho toka City.

Arsenal kuanza kwao mechi katika uwanja wao wa nyumbani wa Emirates kunawapa imani zaidi ya kuanza vyema msimu huu wa ligi na pengine Wenger kujaribu kuwapa Guners kile alichowapa 2004.

No comments:

Post a Comment

Adbox