Katika kuhakikisha kero ya Maji inakwisha kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Shirika la Majisafi naMajitaka jijini Dar es salaam (DAWASCO) limezindua vizimba 8 vya Majisafi katika mtaa wa Mvuleni uliopo katika kata ya Manzese wilaya ya Kinondoni, ili kuwapunguzia wakazi wa maeneo hayo adhaa ya kutafuta Majisafi na salama kutoka umbali mrefu baada ya kuyakosa kwa takribani miaka 30.
Akizungumza katika uzinduzi huo wa vizimba vya Majisafi, Meneja wa Dawasco mkoa wa Magomeni, Mhandisi Pascal Fumbuka, ameeleza kuwa wameamua kufikisha huduma ya Majisafi katika mtaa huo wa Mvuleni kwa njia ya kujenga vizimba vya Majisafi kutokana na eneo hilo kutoingilika kimtaa, hivyo kupelekea kushindwa kuweka mabomba ya Majisafi ya nyumba kwa nyumba.
Aidha, Mhandisi Fumbuka ameongeza kuwa, wapo kwenye jitihada za kuongeza mradi mdogo wa bomba la inchi 6 ambalo litasaidia kuongeza msukumo wa Majisafi ili kuwahudumia wakazi wengi zaidi wa maeneo hayo ya Mvuleni pamoja na mitaa jirani ya Muungano na Kilimani.
“Katika kutatua kero ya Maji hapa Manzese Mvuleni, tumejenga vizimba vya Majisafi nane na tunatarajia wakazi zaidi ya elfu thelathini na sita watanunufaika na vizimba hivi. Tumeshindwa kufikisha bomba kwa kila mkazi kutokana na ujenzi holela wa makazi ya watu, lakini tuamini kuwa vizimba hivi vitasaidia kuondoa kero ya Maji kutokana na msukumo wake wa Maji kuwa mkubwa, hivyo tunaamini havitaleta msongamano pamoja usumbufu kwa wakazi pale watakapokuwa wanakinga Maji” alisema Mhandisi Fumbuka.
Kwa upande wa mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mvuleni Bw. Mrita Mzee ameishukuru Dawasco kwa kujenga vizimba hivyo vya Majisafi kwani wakazi wa mtaa wake walikuwa wakipata adhaa ya kutafuta Majisafi na salama kutoka umbali mrefu na kwa muda mrefu, amewataka wananchi kuvitunza pamoja na kuvilinda vizimba hivyo vya Majisafi ili viweze kuwasaidia kwa kipindi kirefu zaidi.
“Nawashukuru sana Dawasco Magomeni na uongozi wake kwa kutukumbuka na kujengea vizimba hivi vya Majisafi, naamini vitaondoa kero ya Maji iliyokuwepo awali na niwaombe tu wananchi kushirikiana kwa pamoja katika kuvitunza na kuvilinda vizimba hivi ili kuepuka kurudi tena katika shida ya Maji tuliyokuwa nayo hapo awali” alisema Bw. Mzee.
Naye, mkazi wa mtaa huo wa Mvuleni Bi. Hawa Mohamed amesema kuwa vizimba hivyo vya Majisafi vimekuwa mkombozi mkubwa kwao kwani wanawake ndio ambao wamekuwa wakihangaika kutafuta Majisafi kwa muda mrefu, hivyo kusababisha kushindwa kufanya shughuli zingine za kimaendeleo. Aidha, ameiomba Dawasco kuongeza vizimba katika sehemu iliyobaki ya mtaa huo ili kuepuka msongamano kwenye vizimba hivyo.
“Vizimba hivi vya Majisafi kwa kweli vimetuokoa sisi wanawake wa mtaa wa Mvuleni maana tulikuwa tunapata shida mno kuyapata na tulikuwa tukiyanunua kwa bei ya juu sana, bei ambayo sisi watu wakawaida ilikuwa inatuwia vigumu kuimudu” alisema Bi. Hawa.
No comments:
Post a Comment