Wakili Tundu Lissu na wenzake wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS)
wamelikomalia vilivyo sakata maarufu la Bashite linalohusiana na tuhuma
za kughushi vyeti vya kielimu linalomkabili mmoja wa wakuu wa mikoa kwa
kulifikisha kortini ili lipatiwe ufumbuzi.
Aidha, Lissu
na wenzake hao wamedhamiria kuona kuwa kigogo huyo anayetuhumiwa
kuliacha jina lake halisi la Daudi Albert Bashite kutokana na matokeo
mabovu ya sekondari na kutumia jina la mtu mwingine, achukuliwe hatua za
kisheria ikiwamo kufungwa jela kwa kosa la kughushi ikiwa itathibitika
kuwa ana hatia.
Akizungumza jana na waandishi wa habari
mjini Dodoma jana, Lissu ambaye ni Rais wa TLS, alisema uamuzi huo wa
kulifikisha mahakamani suala la Bashite umetokana na maazimio ya baraza
la uongozi la chama hicho, lengo likiwa ni kulinda utawala wa sheria na
uwajibikaji nchini.
Tofauti na matarajio ya baadhi ya
watu, sakata hilo la Bashite halikupatiwa jibu kutokana na ripoti ya
uhakiki wa vyeti vya watumishi wote wa umma iliyokabidhiwa kwa Rais John
Magufuli Ijumaa kutowagusa viongozi wa kisiasa wakiwamo mawaziri, wakuu
wa mikoa, wabunge na madiwani.
Katika kufanikisha nia
hiyo ya TLS, Lissu aliyekuwa na viongozi wengine wa chama hicho wakiwamo
Makamu Rais, Godwin Ngwilimi na Wakili Stephen Kuwayawaya, alisema
miongoni mwa hatua walizochukua ni pamoja na TLS kufungua mashtaka
binafsi ya jinai dhidi ya mkuu huyo anayedaiwa kuitwa Bashite.
Aliongeza kuwa mkuu huyo wa mkoa, anatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya
jinai likiwamo hilo la kutumia vyeti feki na kwamba, kazi ya kumshtaki
haitachukua miezi bali ni wiki mbili au tatu.
“Kifungu
cha 128(2) cha sheria ya Mwenendo wa jinai, sura ya 20 ya sheria za
Tanzania kinaruhusu mtu binafsi (pamoja na taasisi, kampuni au mashirika
kama TLS) kupeleka malalamiko kwa hakimu mwenye mamlaka pale anapoamini
kuna sababu za msingi zinazoonyesha kuwa kosa la jinai
limetendwa,”alisema Lissu, akielezea vifungu wanavyotumia kufikisha
suala hilo kortini.
Alisema dhana ya utawala wa sheria
ina maana pana na kwamba, pamoja na mambo mengine, siyo tu kwamba hakuna
mtu aliyeko juu ya sheria, bali pia kila mtu bila kujali cheo au nasaba
na hali yake kiuchumi na jamii, yuko chini ya udhibiti wa sheria za
kawaida za nchi na hivyo yuko pia chini ya mamlaka ya mahakama za
kawaida.
“Kuna tuhuma za muda mrefu sasa kwamba Mkuu huyo
wa mkoa ametumia vyeti vya shule ya sekondari visivyokuwa vyake. Yeye…
ni Daudi (Albert) Bashite,” alisema Lissu, akiongeza kuwa jina
linalotumiwa sasa na mkuu huyo linadaiwa kuwa mwenyewe yupo na ndiye
mwenye vyeti halisi, na kitendo hicho ni kosa la jinai.
Akifafanua zaidi, Lissu alisema kifungu cha 120 cha Kanuni ya Adhabu,
Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania, kinasema “Mtu yeyote aliye kwenye
utumishi wa umma ambaye, wakati akitekeleza majukumu ya ofisi yake
akifanya kitendo cha udanganyifu au ukiukaji dhamana huo ungekuwa ni
kosa la jinai kama ungefanywa na mtu binafsi au la, anafanya kosa na
endapo atapatikana na hatia atapata adhabu ya kifungo cha miaka saba
jela.”
Lissu alisema kwa kutumia vyeti vya shule
visivyokuwa vyake, na kwa kutumia majina ya mtu mwingine wakati akiwa
mtumishi wa umma, mkuu huyo mwenye jina halisi la Daudi Bashite
ameathiri imani ya wananchi kwa serikali yao kwa kuajiri na kulinda watu
wadanganyifu na wasiokuwa na vyeti halali.
“Mtu huyu
amefanya kosa la jinai ambalo kwalo anastahili kushtakiwa mahakamani na
endapo atapatikana na hatia anastahili kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria
za kawaida za nchi yetu,” alisema Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema).
Lissu aliongeza kuwa endapo
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) atakataa kutoa ridhaa, TLS itamfungulia
mkuu huyo wa mkoa mashtaka ya rejea ya kimahakama katika Mahakama Kuu
ili alazimishwe kutoa ridhaa hiyo.
Kabla ya kumkabidhi
Rais Magufuli ripoti ya uhakiki wa vyeti vya elimu na kitaluma kwa
watumishi wa umma nchini, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na
Uatawala Bora, Angela Kairuki, alisema watumishi 9,932 walikutwa na
vyeti vya kughushi na kwamba, ripoti hiyo haikuwagusa viongozi wa
kisiasa wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge na
madiuwani.
Hata hivyo, Makamu Rais wa TLS, Ngwilimi,
alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha Sheria ya Utumishi wa Umma namba 3
na 5, tafsiri ya mtumishi wa umma inawahusisha pia Wakuu wa mikoa na
Wakuu wa Wilaya na hivyo kina Bashite walipaswa pia kuhusishwa katika
uhakiki huo.
Source:Mpekuzi
Monday, May 1, 2017
Home
/
HABARI MBALIMBALI
/
Tundu Lissu Akomalia Vyeti FEKI Vya Bashite........Aungana na Wanasheria Wenzake Kufungua Kesi Mahakamani
Tundu Lissu Akomalia Vyeti FEKI Vya Bashite........Aungana na Wanasheria Wenzake Kufungua Kesi Mahakamani
Tags
# HABARI MBALIMBALI
About Unknown
Soratemplates is a blogger resources site is a provider of high quality blogger template with premium looking layout and robust design. The main mission of templatesyard is to provide the best quality blogger templates.
HABARI MBALIMBALI
Labels:
HABARI MBALIMBALI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


No comments:
Post a Comment