Thursday, March 30, 2017

KIWANDA CHA MAFUTA KISIWANI PEMBA KUWEKA KIFAA MAALUMU CHA KUFYONZA KEMIKALI

 
UONGOZI wa Kiwanda cha mafuta ya makonyo, kilichopo Wawi wilaya ya Chakechake kisiwani Pemba, umesema moshi unaotoka kwenye kiwanda hicho, hauna madhara makubwa kwa sasa, baada ya kuwekea kifaa maalum ya kufyonza kemikali zinazoathiri afya ya mwanadamu.
 
Akizungumza na wajumbe wa Tume ya kurekebisha sheria iliokuwa chini ya Mwenyekiti wake Jaji Mshibe Ali Bakari, Meneja uzalishaji wa kiwanda hicho Habibu Mohamed Ali, alisema baada ya wahindi kukijenga upya kiwandha hicho, walifanikiwa kuweka kifaa maalum cha kuondosehea madhara.
 
Aidha Meneja huyo uzalishaji, aliwaambia wajumbe wa tume hiyo kuwa, licha kuwepo kwa kifaa hicho kinachochuja baadhi ya madhara, pia wamefanikiwa kuurefusha mlingoti unaotoa moshi kwa kwenda juu zaidi.
 
Ujumbe wa Tume hiyo ya kurekebisha sheria, ulifika kwenye kiwanda hicho, ili kuangalia mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na usalama wa wafanyakazi na suala la fidia, wakati huu wakizifanyia mapitio sheria za fidia na ile ya usalama kazini za mwaka 2005.
Katika hatua nyengine Meneja huyo uzalishaji kiwandani hapo, aliuhakikishia ujumbe huo kuwa, wako katika mikakati na mipango ya kuhakikisha kiwanda hicho, kinazalisha na hakiathiri afya za wafanyakazi wake na wananchi kwa ujumla.
 
Mapema Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar Jaji Mshibe Ali Bakari, alisema hakuna uhusiano kisheria baina ya kuwepo kiwanda na kuathiri afya za wafanyakazi na wananchi wengine.
 
Kwa upande wao wanasheria wa tume hiyo, waliuomba uongozi wa kiwanda hicho, kuzielewa sheria za fidia na ile ya usalama kazini, ili kuwafundisha wafanyakazi wao.
Nao wafanyakazi wa Kiwanda hicho, walisema hawazifahamu sheria za kazi wala za fidia, na ikitokezea mtu amepata athari inayotokana na kazi hiyo, hujitibu kwa gharama zake.
Suleiman Juma ambae ameanza kazi kiwandani hapo zaidi ya miaka 20 sasa, alisema aliwahi kuungua na kufikishwa hadi hospitali ya Muhimbili kwa gharama zake.
“Mimi sujui kuwa ukipata madhara kazini au kutokana na kazi yako, muajiri ndie anaepaswa kugharamia matibabu, lazima tuelimisha sheria hizi za kazi’’,alifafanua.
Mara baada ya mazungumzo hayo, wajumbe wa tume hiyo walikagua sehemu mbali mbali za kiwanda hicho kilichojengwa mwaka 1982, ikiwa ni pamoja na eneo za uzalishaji na shamba la mimea Mtakata lililopo Wawi.

No comments:

Post a Comment

Adbox